HABARI KUU
Sita wahofiwa kufa tukio la daraja kuporomoka Marekani
Huku shughuli ya kuwatafuta ikiendelea wafanyakazi sita waliotoweka baada ya Daraja la Francis Scott Key mjini Baltimore, Marekani kuporomoka jana Jumanne wanahofiwa kuwa wamefariki dunia.
Mkuu wa polisi wa Jimbo la Maryland Roland L. Butler Jr., amesema Jumanne jioni kuwa operesheni ya utafutaji na uokozi sasa inabadilishwa kuwa ya utafutaji wa miili.
Amesema wapiga mbizi watarejea katika eneo la tukio asubuhi (kwa saa za Marekani) kwani mazingira ya usiku yalikuwa magumu kidogo kwao.
Meli kubwa ya shehena iligonga nguzo ya daraja hilo na kusababisha kuvunjika vipandevipande na kutumbukia majini.
Gavana wa Maryland amesema wahudumu wa meli hiyo walituma ujumbe wa dharura wa kuomba msaada muda mfupi kabla ya tukio hilo kutokea, hatua iliyowasaidia maofisa kupunguza idadi ya magari kwenye daraja hilo.