Habari Kuu
Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini amewasili nchini Urusi kwa ziara ya nadra nje ya nchi siku moja baada ya mataifa hayo mawili kudhibitisha uvumi kuwa Kim atakutana na Vladimir Putin katika siku za karibuni.
Treni ya kisasa ya kijani kikavu ilionakishiwa kwa ufito wa rangi ya dhahabu ,ilivuka mpaka wa Korea Kaskazini na kuingia upande wa mashariki mwa Urusi ikiwa imembeba Kim na ujumbe wake.
Iliondoka Pyongyang, mji mkuu wa Korea Kaskazini siku ya jumapili ,ambapo Kim aliagwa kwa heshima zote na maafisa wake wa ngazi za juu. Picha za kwanza za safari hiyo ,zimetolewa leo na shirika la habari la nchi hiyo. Kiongozi huyo anatarajia kukutana na Putin katika eneo ambalo hadi sasa alijatajwa lakini inaaminika itakuwa ,upande wa mashariki ya mbali ya nchini Urusi.
Rais Vladimir Putin hivi sasa yuko kwenye mji wa Vladvosto ulio jirani na Korea Kaskazini kuhudhuria jukwaa la kiuchumi la mataifa ya Mashariki. Hata hivyo hakuna ishara kwamba Putin atakutana na Kim kwenye eneo hilo. Duru zinasema ,Putin anapanga kusafiri kwenda kwenye eneo jingine liitwalo Vschocomentome na ndio pengine atakutana na Kim.
Wakati wa hotuba yake na hata kwenye mjadala wa wazi mkutano wa Vlazvostocky,Putin hakusema lolote kuhusu mkutano wake na Kim na badala yake alirejea matamshi yake ya kuyalaumu mataifa ya Magharibi kwa hali ya kiuchumi Duniani na matatizo mengine yanayoukabili Ulimwengu
“Sote tunafahamu na sote tunaona jinsi uchumi wa Dunia ulivyobadilika na unavyoendelea kubadilika miaka ya karibuni na pia hilo ni kutokana na ukweli, baadhi ya mataifa hususan ni ya Magharibi ndio yanaharibu kwa mikono yao wenyewe mfumo wa kifedha ,biashara na ushirikiano wa uchumi ambao waliubuni na kuupigia chapuo”
Mkutano wake na Kim ,wafatiliaji wanasema Putin huenda ataomba kupatiwa mabomu na makombora ya kuchakaza vifaru vya kivita kutokea Korea Kaskazini, huku Pyongyang itaweka mezani maombi ya kupatiwa msaada wa teknolojia hili kaunda satellite ya kisasa na nyambizi zinazotumia nishati ya nyuklia.
Marekani ambayo wiki iliopita ilidokeza kwa mara ya kwanza Mipango ya mkutano wa Kim na Putin ,imeitahadhalisha Korea Kaskazini kuwa italipa iwapo itaipatia Urusi silaha kwaajili ya vita nchini Ukraine. Imezikumbusha nchi zote mbili kwamba upelekaji wowote wa silaha za Korea Kaskazini nchini Urusi, utakuwa ni ukiukwaji wa maazimio kadhaa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Baada ya miongo kadhaa ya mahusiano ya panda shuka ,Urusi na Korea Kaskazini zimejongelea sana tangu Moscow ilipotuma vikosi vyake nchini Ukraine mnamo mwaka 2022. Mshikamano wao unatokana na dhamira ya Kim ya kuimarisha mahusiano na washirika wake wa jadi ambao ni Urusi na China huku ikijaribu kujitoa kimasomaso baada ya kutengwa na Ulimwengu