HABARI KUU
Kumekuwa na sintofahamu nchini Kenya baada ya Rais wa Angola Joâo Lourenćo kutokuhudhuria sherehe za Mashujaa Day Nchini Kenya kama ilivyotarajiwa licha ya kuwasili nchini humo.
Mtandao wa “Daily Nation ” umeripotiwa kuwa Waziri Mkuu, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya,Musalia Mudavadi ,wakati akimpokea mgeni huyo aliyeambatana na mkewe Ana Dias Lourenço,alidokeza kuwa ndiye aliyealikwa kuwa mgeni wa heshima katika sherehe hizo.
Rais huyo wa Angola 🇦🇴 aliwasili Kenya siku ya Alhamisi ambapo ilitarajiwa afike Kericho ambako ndiko sherehe hizo zilifanyika kitaifa, huku akitarajiwa kuwa mgeni wa heshima kwa mujibu wa mawasiliano rasmi kati ya Kenya na Angola 🇦🇴.
Hata hivyo jana Ijumaa Oktoba 20,2023 katika programu rasmi ya “Mashujaa Day ” haikuorodhesha uwepo wa Rais Lourenço kama mgeni rasmi ,badala yake aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola Balozi António Tete.
Katika hotuba yake ,Balozi António Tete amesema kutokuwepo kwa Rais Lourenço kumetokana na “sababu zisizotarajiwa” na hivyo kuwaomba radhi Wakenya kwa niaba ya Rais wake.
“Kwa niaba ya Rais Joáo Lourenço kwanza ningependa kuomba radhi kwa kutokuhudhuria sherehe hizi. Angependa kuwa pamoja nanyi lakini kwasababu ya sababu zisizotarajiwa, hakufika Kericho
“Hata hivyo,anawatakia kheri mnaposheherekea siku hii ya leo muhimu, pia anawashukru kwa mapokezi mnayotupa tunapokuja Kenya 🇰🇪 “
Amesema balozi Tete
Katika hotuba yake wakati wa sherehe hizo, Rais William Ruto amesema kuwa Rais Lourenço bado yuko nchini humo na kwamba atakuwa na ziara ya kiserikali leo jumamosi.
“Tunapozungumza sasa, Rais Joáo Lourenço wa Angola bado yuko Kenya 🇰🇪, na atakaribishwa katika ziara ya kikazi kuanzia kesho jumamosi “.
Amesema Rais William Ruto.
Hadi jana jioni, Ikulu ya Kenya ilikuwa imekwishatuma mwaliko kwa vyombo mbalimbali vya habari ili kuhabarisha umma juu ya ziara ya kiserikali ya jumamosi.