HABARI KUU
Mapambano ya kukabiliana na ujangili wa Faru nchini Afrika Kusini yamechukua sura mpya baada ya idadi ya faru waliouawa kuongezeka mwaka 2023.
Mwaka jana faru 499 waliwindwa, ikiwa ni ongezeko la faru 51 kutoka mwaka uliopita, amesema Waziri wa Mazingira wa Afrika Kusini Barbara Creecy.
Afrina Kusini ina faru wengi zaidi duniani.
Nchi hiyo ina faru 2,000 weusi, ambao wanadhaniwa kuwa hatarini zaidi kutoweka na takriban faru weupe 13,000 ambao nao pia wanakaribia kuwa hatarini kutoweka.
Ujangili ulipungua sana kuanzia mwaka 2014, lakini kasi imeongezeka hivi karibuni.
Pembe za faru zina soko kubwa katika mataifa ya Asia, kama vile China na Vietnam ambapo hutumika kutengenezea dawa za kienyeji.
Wengi wa faru waliouawa mwaka jana ni kutoka hifadhi ya Hluhluwe-iMfolozi iliyopo KwaZulu-Natal.
Hifadhi kubwa zaidi ya Afrika Kusini, Kruger, ambayo zamani ilikuwa kitovu cha ujangili, ilishuhudia kupungua kwa ujangili kwa zaidi ya theluthi moja mwaka 2023.
Mafanikio ya kupambana na ujangili Kruger, yamesababisha makundi ya uhalifu kwenda kwenye hifadhi nyingine, Bi Creecy aliwaambia waandishi wa habari.