HABARI KUU
Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) kimepokea jumla ya shilingi bilioni 73.6 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa HEET.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda amesema fedha hizo zimetumika katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na upanuzi wa miundombinu, mapitio ya mitaala, ununuzi wa vifaa vya kuboresha maabara, karakana, na mashamba ya mafunzo, pamoja na kuongeza ushirikiano na Mataifa mengine.
Amesema, wamesaini makubaliano na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kuwapata wataalamu wa kilimo wenye sifa kwa miradi mbalimbali, na kwa sasa vijana 300 wanafanya kazi ya Maafisa Ugani katika Mikoa mbalimbali Nchini.
“Kwasbabu tumeingia makubaliano na wizara ya kilimo na kuna mambo ambayo tumeyaainisha na kuyabaonisha ambayo yatakuwa majukumu ya chuo cha kilimo moja wapo kama nilivyosema mwanzo sisi tunawasaidia kwenye kutafuta,kuchuja vijana ambao tunaamini wanaweza kuwa sehemu ya huo mradi,” amesema Chibunda.
Hata hivyo, SUA inajivunia Mafanikio makubwa ya ongezeko la idadi ya Wanafunzi Chuoni, ambapo katika miaka mitatu iliyopita kumekuwa na ongezeko la zaidi ya Wanafunzi 3800 kutoka nchini na baadhi yao kutoka mataifa mengine Duniani.