MICHEZO
Kocha mkuu wa klabu ya Singida Fontaine Gate Fc, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ametupilia mbali taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ametimka klabuni hapo baada kuiongoza kwa mechi mbili tu tangu apewe kibarua cha kuiongoza klabu hiyo kwenye mechi 10 zilizosalia za Ligi.
Akizungumza juu ya taarifa hizo Julio amesema hafahamu chochote kuhusu taarifa hizo huku akibainisha kuwa ikiwa kuna chochote kuhusu yeye kuondoka Singida, basi klabu hiyo au yeye mwenyewe ataweka wazi.
Julio alitua Singida Fontaine Gate mnamo Machi 13, 2024 kwa kandarasi la kukinoa kikosi hicho mpaka mwisho wa msimu 2023/24 ambapo alipewa ajenda 10 za kuiongoza klabu hiyo kwenye mechi 10 za mwisho za Ligi.
Mpaka sasa Julio ameiongoza Singida FG kwenye mechi mbili huku akishinda mechi moja (ushindi wa 1-0 dhidi ya Namungo kwenye Ligi Kuu) na kipigo cha 3-0 dhidi ya Tabora United kwenye kombe la Shirikisho la CRDB.