NYOTA WETU
Mwenyekiti na Mfadhili wa zamani wa Young Africans, Yusuf Manji amesema kwa sasa hafikirii kurejea ndani ya klabu hiyo ingawa anafurahia kuona imekuwa na umoja na mshikamano wa hali ya juu.
Manji amesema kwa sasa umri wake unambana kujiweka karibu na timu hiyo na soka kwa ujumla, hivyo anaendelea kujishughulisha na mambo mengine.
“Kwa sasa siwezi, kwanza umri umeenda siwezi zile pilikapilika za kusimamia timu,” amesema Manji aliyeiongoza Young Africans kwa miaka minne.
“Unajua hata kama utakuwa ofisini, tabia yangu ni kwamba napenda kufanya kazi zote nikiwa karibu. Naweza kuwa na viongozi wengine lakini nitalazimika kusafiri na wachezaji, nahakikisha kila kitu chao kinaenda vizuri, ukweli kwa kipindi hiki sitakuwa na uwezo tena wa kufanya hivyo wanatakiwa kufanya vijana.”
Manji amesema kuwa pamoja na hilo, anafurahia kuona klabu hiyo ina umoja wa hali ya juu kwa sasa jambo ambalo lilikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu.
“Moja ya jambo ambalo nakumbuka nililifanya na kuisaidia Young Africans hii kufika hapa ni kuweka umoja, wakati naingia nilikuta migogoro mingi kulikuwa na makundi matatu, nakumbuka moja liliitwa Yanga Asili, lingine Kampuni moja liliitwa Yanga Akademia.
“Nilitumia ushawishi na wangu wote na kuhakikisha haya makundi yanaisha na Young Africans ikasimama, nafikiri imewasaidia hadi leo ndiyo maana kuna umoja,” amesema Manji.
Katika hatua nyingine Yusuf Manji amefunguka sakata la mashabiki kuingia uwanjani bure
“Nilianzisha mfumo wakati mwingine wa kununua tiketi zinaenda kugawiwa kwenye matawi ya Young Africans kwa kuwa nilitaka kurudisha kwa jamii. Kama unakumbuka mchezo wa Young Africans na TP Mazembe mashabiki waliingia bure.”
“Pale haikuwa bure kama ambavyo inafanyika sasa, bali nilinunua tiketi zote zikagawiwa kwa mashabiki wa Young Africans kupitia kwa viongozi wa matawi yao. Nia ilikuwa ni kuhakikisha mchezo huu unarudi kwa jamii yetu,” amesema Manji mmoja wa wafadhili wa klabu walioweka rekodi ya kuwa kipenzi cha mashabiki nchini.”
Related Content