MICHEZO
Uongozi wa Klabu ya Liverpool utakuwa na upinzani mkali kutoka kwa FC Bayern Munich, katika vita ya kuiwania saini ya Kocha wa Klabu ya Feyenoord ya Uholanzi Arne Slot.
Meneja wa Bayern Thomas Tuchel ataondoka mwishoni mwa msimu huu 2023/24, baada ya mambo kumuendea vibaya na tayari uongozi umeshafikia makubaliano ya kuachana naye.
Gazeti la The Independent la England limeripoti kuwa Kocha Slot yuko tayari kuanza mazungumzo na Uongozi wa Liverpool.
“Liverpool wamefanya mazungumzo na Feyenoord kwa ajili ya Arne Slot baada ya kumtambua Mholanzi huyo kama mgombea wanayempendekeza kuchukua mikoba ya Jurgen Klopp.
“Slot, ambaye alishinda Kombe la Uholanzi juma lililopita na Eredivisie msimu uliopita, amebakiza miaka miwili katika mkataba wa miaka mitatu aliousaini msimu uliopita.
“Liverpool inaweza kukabiliana na ushindani kwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 kutoka FC Bayern Munich huku Slot akiibuka kama mshindani wa kazi kadhaa kuu ambazo zitatolewa msimu huu wa joto.
“Liverpool wametathmini wasifu wa makocha mbalimbali, huku Ruben Amorim wa Sporting Lisbon akiwa mstari wa mbele baada ya kuwavutia viongozi wa klabu hiyo, huku chaguo lao la kwanza Xabi Alonso, akikataa kuondoka Bayer Leverkusen.”