HABARI KUU
Raia wengi wa Iran wamejitokeza katika mji mkuu wa nchi hiyo Tehran, kushiriki katika mazishi ya kitaifa ya Rais Ebrahim Raisi.
Rais huyo wa Iran akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Hossein Amir – Abdollahian pamoja na maafisa wengine sita wa ngazi ya juu, walifariki dunia baada ya helikopta waliyokuwa wakisafiria kuanguka karibu na eneo la mpaka wa Iran na Azerbaijan.
Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei ataongoza dua mjini Tehran kabla ya majeneza yaliyobeba miili ya viongozi hao kupelekwa katika uwanja mkubwa wa Azadi, ambapo yatafanyika mazishi hayo ya kitaifa.
Picha mbalimbali za video zilizorushwa kupitia kituo cha televisheni cha Serikali ya Iran zimeonyesha mitaa mbalimbali ya Tehran ikiwa imejaa waombolezaji, wengi wao wakiwa wamebeba picha ya Rais Raisi na wengine wakiwa wameshika bendera za Taifa hilo.
Viongozi kutoka mataifa mbalimbali wamethibitisha kushiriki kwenye mazishi hayo ya kitaifa ya Rais huyo wa Iran.
Baada ya mazishi hayo ya kitaifa mjini Tehran, mwili wa Rais Ebrahim Raisi utasafirishwa kwenda jimbo la Khorasan ambalo lipo kusini mwa Iran na baadae nyumbani kwake Mashhad kwa ajili ya mazishi rasmi yatakayofanyika kesho Alhamisi Mei 23, 2024.