Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi ameiahidi mahakama kutoa ushirikiano ili kukamatwa kwa basi la Kampuni ya Mabasi ya Kilimanjaro (Kilimanjaro Express) lenye namba T 178 EAU, baada ya kusababisha kifo cha Immaculate Kisena (16) aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha tano.
Kitinkwi amefika katika Mahakama Kuu, Kanda la Dar es Salaam, baada ya kupata wito wa mahakama ili ajieleze kwa nini alikiuka amri ya mahakama ya kukamatwa kwa gari hilo lililotakiwa liuzwe ili familia ya Leonard Kisena ilipwe fidia.
Katika maelezo yake mbele ya Msajili wa Mahakama hiyo, Sundi Fimbo, Kamanda Kitinkwi amedai kuwa alipokea simu kutoka kwa abiria waliokuwa wakisafiri na basi hilo wakilalamika kuzuiliwa kuendelea na safari eneo la Shekilango, Dar es Salaam na kudai kuwa kibinadamu aliwaruhusu abiria waendelee na safari kwa sababu kuepeleka basi lingine kwa wakati huo ilikuwa ngumu.
“Kwa sababu magari huwa yanakaguliwa kabla ya kuanza safari, kwa hivyo nikaona kuruhusu gari lingine ambalo halijakaguliwa ingeleta shida. Nikaruhusu liende halafu kesho yake (Mei 16, 2024 ) saa saba mchana lipelekwe Kituo cha Polisi Oysterbay,” amedai RPC Kitinkwi
Hata hivyo, baada ya kutoa maelezo hayo ameahidi kuwa atatoa ushirikiano ili kukamatwa kwa basi hilo na kurudishwa kwa dalali wa mahakama huku Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Rolinda Sawaya akidai kuwa yeye hakuhusika kuzuia basi kuendelea na safari kwa kuwa yeye hajui mambo ya sheria.
Kufuatia maelezo hayo, Msajili Fimbo ametoa amri kuwa utekelezaji wa kukamatwa kwa gari zenye namba T 178 EAU na T 508 DDB uendeee kisha dalali apeleke mrejesho kwa mahakama ili aweze kupata ruhusa ya kuyauza magari hayo.
Akizungumza nje ya mahakama, Wakili wa wadai hao, Mngumi Samadani amedai kuwa mahakama hiyo ilifikia hatua hiyo, baada ya kuwasilisha hoja mahakamani kutokana na dalali wa mahakama kuzuiliwa kukamatwa kwa gari hilo wakati tayari mahakama ilishatoa amri.
Awali, akisoma hukumu kwa niaba ya Jaji Leila Mgonya, Msajili wa Mahakama Kuu, Joseph Luambano alisema wadaiwa wote wanatakiwa kulipa fidia ya Sh milioni 300 kwa kusababisha kifo, majeruhi na uharibifu wa gari hilo.
Kisena ambaye ni baba mzazi wa marehemu, Desemba 24, 2021 akiwa na watoto wake wawili na mke wake wakiwa safarini kuelekea mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya basi la Kilimanjaro liliacha njia na kuwagonga na kusababisha kifo cha mtoto wake papo hapo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 3,2024.