Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka waganga wakuu wa mikoa, waganga wakuu wa wilaya pamoja na waganga wafawidhi wa hospitali kwa ngazi zote nchini kuzingatia maelekezo ya mwongozo wa kutozuia maiti na kuweka utaratibu wa kulipia gharama za matibabu na madeni ya miili ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma pasipo kuwepo kwa vikwazo vinavyochelewesha marehemu kuzikwa.
Dkt. Mollel amebainisha hayo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya wabunge katika bunge la 12 mkutano wa 15 kikao cha 38.
“Serikali ilishatoa maelekezo kwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kupitia waraka namba moja wa mwaka 2021 wa kutozuia maiti na kuweka utaratibu wa kulipia gharama za matibabu na madeni ya miili”. Ameeleza Dkt. Mollel
Aidha, amesema madhara anayoweza kupata mtoto anapozaliwa na kuchelewa kulia ni kuathirika kwa ubongo ambapo hupelekea kupata mtindio wa ubongo, kuchelewa kwa hatua za makuzi na maendeleo ya mtoto kama vile kuchelewa kukaa, kutembea na kuongea na kutochangamana na wenzake au kutokucheza na wenzake.
“Nitoe wito kwa kila mjamzito kuanza kliniki mapema mara tu anapogundulika kuwa na ujauzito sambamba na kuhakikisha wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma ili ikiwa kuna tatizo la uzazi pingamizi watoa huduma waweze kuwasaidia mapema kabla mtoto hajaathirika”. amesema Dkt. Mollel.
Related Posts 📫
Discover more from JUNIITV.ONLINE
Subscribe to get the latest posts sent to your email.