Baada ya miaka kadhaa ya kusubiri njia mbadala za uzazi wa mpango kwa Wanaume, Watafiti wamesema hatimaye wamepiga hatua kubwa katika chaguo mahususi kwa ajili ya Wanaume ambapo bidhaa ya majaribio ya uzazi wa mpango ambayo ipo kwa mfano wa mafuta (gel) itakuwa ikipakwa na Wanaume kwenye mabega yao mara moja kwa siku na kisha baada ya hapo itakuwa ikizuia uzalishaji wa mbegu za kiume.
Kituo cha Televisheni cha CNN kimeripoti kuwa dawa hiyo ya kupaka imetengenezwa na Taasisi za Kitaifa za Afya na Baraza la Idadi ya Watu nchini Marekani ikichukua mbinu sawa na njia za kudhibiti uzazi kwa Wanawake ambapo itatumia homoni mbili ambazo ni nestorone na testosterone.
CNN wameripoti kuwa geli hiyo itawasaidia Wanaume kukaa kwenye hali nzuri ya kiafya lakini mbegu zao hazitokuwa na nguvu za kutosha kumpa Mwanamke ujauzito ambapo Watafiti hawa wamekuwa wakitengeneza na kuboresha dawa hiyo tangu mwaka 2005 huku jaribio walilolifanya hivi karibuni likihusisha zaidi ya Wanandoa 300 ambao uzalishazi wao wa mbegu za kiume ulipungua.
Watafiti hao wamesema ikiwa Mwanamke atasahau kidonge za uzazi wa mpango kwa siku moja au mbili, anaweza kuepuka mimba zisizotarajiwa pale ambapo Mwenza wake atapaka hiyo dawa mabegani ambapo utafiti umeonesha pia kuwa mbegu za kiume zitaweza kuongezeka nguvu kwenye muda wa wiki 8 hadi 10 baada ya Mwanaume kusitisha matumizi ya dawa hiyo.
Iwapo Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani itaruhusu matumizi ya dawa hiyo, itafanyiwa majaribio ya mwisho mwaka 2025.