Mbunge wa Kisesa (CCM) Luhaga Mpina ambaye anatumikia adhabu ya kutohudhuria vikao 15 vya Bunge, amesema anatarajia kupeleka mahakamani malalamiko yake ya kuondolewa Bungeni kwa kile alichodai kuwa kuna uonevu na kutokutendewa haki na Spika wa Bunge, Tulia Ackson.
Akizungumza alipokutana na Wanahabari jana Juni 29, 2024, Mpina ameongeza kuwa atawafikisha Mahakamani Waziri Bashe na Bodi ya Sukari chini ya lbara ya 26 na 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kitendo cha kutoa idhini ya vibali vya kuagiza sukari kinyume cha Sheria na kulisababishia Taifa hili hasara kubwa.
Vilevile Mpina amesema atayafikisha Mahakamani makampuni yote yaliyojihusisha na uingizaji wa sukari Nchini kinyume cha Sheria.
Baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumpa adhabu Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina ya kutokuhudhuria vikao 15, ametangaza kupeleka malalamiko yake katika vyombo vya sheria akidai kuondolewa Bungeni kwa uonevu na kutokutendewa haki pamoja na kuahidi kumpeleka Mahakamani Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe na Bodi ya Sukari na kuyafikisha Mahakamani makampuni yote yaliyojihusisha na uingizaji wa sukari nchini kinyume na sheria.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam Mh. Mpina amesema hakuna cha kumkatisha tama, na kuahidi kuendeleza mapambano.
“Baada ya kutafakari kwa kina mazingira na kilichotokea kwenye Kamati ya Bunge nimeamua yafuatayo moja kupeleka malalamiko yangu yakuondolewa Bungeni kwa uonevu na Spika wa Bunge kwenye vyombo vya sheria ili vikapime na kutoa haki kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria za Nchi, pili kumpeleka Mahakamani Waziri wa Kilimo, hussein Mohamed Bashe na Bodi ya Sukari chini ya ibara ya 26 na ibara ya 27 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kitendo cha kutoa idhini ya vibali vya kuagiza sukari kinyume cha sheria na kulisababisha Taifa hili hasara kubwa tatu kuyafikisha Mahakamani makampuni yote yaliyo jihusisha na uingizajiwa sukari nchini kinyume na sheria” Amesema Luhaga Mpina