Katika hali isiyo ya kawaida mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina Frola Samson (12), mkazi wa wilaya ya Ilemela amepatikana baada ya msako wa Jeshi la polisi Mkoani Mwanza akiwa eneo la Buhongwa ambako alijificha yeye na mdogo wake aitwaye France Samson (8) huku akidanganya kuwa wametekwa na kutaka wazazi watume fedha ili waachiwe.
Inadaiwa kuwa watoto hao walitoweka nyumbani mnamo tarehe 4.7.2024, ambapo Frola aliiba pesa za Mama yake kiasi cha shilingi 150,000/= na kisha kutoweka na mdogo wake wakielekea Buhongwa ambako alianza kupiga simu kwa Mama yake mzazi akidai atumiwe pesa kwa ajili ya waliowateka ili wawaachie huru.
Hata hivyo Jeshi la Polisi mkoani humo baada ya kupokea taarifa na kufanya ufuatiliaji, limefanikiwa kuwapata watoto hao wakiwa salama huku wakiwa na simu, godoro na vyombo vingine vya matumizi ya ndani walivyonunua kwa kutumia pesa aliyoiba mtoto huyo.