Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshitakiwa kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania iliyopo Dar es Salaam kuhusu tukio la kuzima mtandao (internet shutdown) wakati wa uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba, 2020.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wakili Tito Elia Magoti anayemwakilisha mdai, shauri hilo la kikatiba limefunguliwa na Kumbusho Dawson Kagine, mtumiaji wa mitandao ya kijamii ambaye pia Katibu Mtendaji wa Reach Out Tanzania.
Tito akiwa na Wakili Mwenza Alphonce Lusako wameeeleza kuwa shauri hilo limefunguliwa kwa maelekezo ya mteja wao ambaye ni Kumbusho dhidi ya Waziri Wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Ni madai ya mteja wetu kwamba mtandao ulizimwa kwa makusudi, na kwamba tukio hilo lilivunja haki kadhaa zinazolindwa na Katiba ya JMT. Mathalani, haki ya kupata, kutoa na kusambaza taarifa (Ib 18), uhuru wa kukutanika na kushirikiana na wegine (lb 20(1)), na uhuru wa kushiriki shughuli za umma (Ib 21(1, 2)), na wajibu wa serikali kuheshimu katiba na sheria za nchi (Ib 26)” Ameeleza Tito.
Aidha ameeleza kuwa haki hizo zimekiukwa katika Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, Mkataba wa Kimataifa unaohusu Haki za Raia na Siasa na Mkataba wa Afrika wa Demokrasia Uchaguzi na Utawala, pamoja na matamko mbalimbali kama Azimio la Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu Kuendeleza, Kulinda na Kufurahia Haki ya Mtandao, Tamko la Afrika Kuhusu Haki ya na wa Uhuru Mtandao la mwaka 2017 na Kanuni za Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kuhusu Uhuru wa Kujieleza Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wakili Tito, Shauri hili litatajwa kwa mara ya kwanza mbele ya Jaji David Ngunyale tarehe 17 Julai 2024 Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam.