Mfanyabiashara wa Ng’ombe wilayani Geita Mkoani Geita, Daniel Sayi(48), anadaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake Kitongoji cha Kiomboi, Kijiji cha Ihilika, Kata ya Nyarugusu mkoani Geita.
Inadaiwa kuwa Sayi alichukuliwa Mei 13,2023 saa 12 jioni baada ya watu wanne waliokuwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye rangi nyeupe kufika nyumbani kwake na kumfunga pingu kisha kumchukua bila kusema chochote.
Kwa mujibu wa familia ya Sayi, wamedai kuwa imepita miezi miwili tangu kuchukuliwa kwake Mei ambapo wamehangaika kumtafuta katika vituo mbalimbali ikiwemo kituo cha polisi Nyarugusu, Katoro na Geita lakini hawajafanikiwa kumpata na hawajui wanaomshikilia ni kina nani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Sophia Jongo alipogiwa simu na wanahabari kuzungumzia tukio hilo, alisema anafuatilia taarifa hiyo kujua undani wake.
“Nataka nifutailie waliliripoti kituo gani na lini? Wakati mwingine kuna kuwa na changamoto mtu anaweza kuripoti akipotea lakini akipatikana harudi tena kumbe alitoka tu na mambo yake wanaona hayupo.” Alisema Jongo.