Mwanamuziki maarufu wa rap, Sean “Diddy” Combs, ameshutumiwa tena kwa ubakaji na unyanyasaji wa kingono katika kundi jipya la kesi tatu zilizowasilishwa Alhamisi katika mahakama kuu ya New York nchini Marekani. Malalamiko hayo yanadai kuwa matukio hayo yalifanyika kati ya mwaka 2019 na 2022.
Shirika la habari la BBC linasema kuwa katika kesi hizo, wanaume wawili wanadai kuwa walihudhuria tafrija iliyoandaliwa na Diddy ambapo walipatiwa vinywaji vya pombe vilivyodaiwa kuwa na dawa za kulevya, na walipoteza fahamu kabla ya kubakwa.
Mawakili wa Diddy wamekanusha vikali madai hayo, wakiyaita “ya uwongo” na wamesema wanapanga kuchukua hatua dhidi ya wanasheria waliowasilisha kesi hizo.
“Tutathibitisha kuwa ni za uwongo na kutafuta vikwazo dhidi ya kila mwanasheria asiye na maadili aliyewasilisha madai haya ya kubuni,” timu ya mawakili ya Diddy ilisema.
Kesi hizi tatu zinajumuika na zaidi ya kesi 30 za madai zilizowasilishwa awali dhidi ya Diddy, nyingi zikiwa zinahusiana na unyanyasaji wa kingono, zikienda nyuma hadi miaka ya 1990. Rapa huyo, ambaye kwa sasa anazuiliwa katika gereza la Metropolitan Detention Center huko Brooklyn, amenyimwa dhamana mara tatu.
Thomas Giuffra, wakili wa wateja waliowasilisha kesi mpya, amesema zaidi ya watu 60 wamewasiliana na ofisi yake na madai dhidi ya Diddy.
“Tumechunguza kwa kina kila moja ya madai hayo na tumeamua kuendelea na kesi hizi tatu kwa sababu tunajua zina ushahidi thabiti,” Giuffra amesema.
Malalamiko haya mapya yanaongeza shinikizo kwa Diddy, ambaye amekuwa akikabiliwa na shutuma zinazohusiana na matumizi mabaya ya nguvu na unyanyasaji kwa miongo kadhaa. Timu ya mawakili wake imeapa kupambana dhidi ya kesi zote, ikisisitiza kuwa tuhuma hizo ni sehemu ya njama za kibiashara na hazina msingi wa kisheria.
Wakati kesi hizi zikisubiriwa kusikilizwa, Diddy bado anakabiliwa na changamoto kubwa za kisheria na kijamii, huku hali ikionekana kuwa mbaya zaidi kwa msanii huyo maarufu.