Tuliokuwepo tutakikumbuka Kikao cha Pili cha Bunge la Kumi Na Moja. Shauku ya tunaofuatilia Siasa za Kibunge ilikuwa ni kuona, ni kwa namna gani Kambi Rasmi ya upinzani ingeundwa. Ni kwa mujibu wa kanuni ya Bunge nr 131.
Historia ni mwalimu mzuri, kazi yangu hapa ni pamoja na kukumbushia historia, maana, wanadamu ni viumbe tulio wepesi wa kusahau.
Mwaka 1995 baada tu ya Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi, CUF iliongoza Kambi Rasmi ya upinzani.
CUF walingia makubaliano na UDP iliyokuwa na wabunge wanne; Isaac Cheyo (Bariadi Magharibi), Danhi Mkanga (Bariadi (Mashariki), Erasto Tumbo (Kisesa) na Teddy Kasela-Bantu (Viti Maalum).
NCCR- Mageuzi walikuwa na wabunge wengi Tanzania Bara kuliko chama kingine cha upinzani. Ni jumla ya wabunge 28.
Ni Wabunge aina ya Mabere Marando; Dk. Masumbuko Lamwai, James Mbatia, Balozi Paul Ndobho, Ndimara Tegambwage na Makongoro Nyerere.
Ni kwenye Bunge la 1995, kambi rasmi ya upinzani Bungeni iliongozwa na mwanamama Fatma Maghimbi, Mbunge wa kuchaguliwa kutoka Chake Chake, Pemba.
Ajabu ya mwaka 1995 CUF katika kuunda kambi rasmi ya upinzani haikuwahitaji NCCR – Mageuzi katika kuimarisha kambi hiyo Bungeni. Hiyo ni pamoja na NCCR-Mageuzi kuwa na kikosi chenye majina ya kutisha aina ya mwanasheria Mabere Marando, Dr Masumbuko Lamwai na hata mwanasiasa machachari wakati huo, Makongoro Nyerere ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa, Songwe.
Mwaka 2000-2005, CUF waliwaalika wabunge wa vyama vingine kuunda kambi ya upinzani kwa kubanwa na kanuni; hawakuwa na wabunge wa kutosha kuunda kambi ya upinzani.
CUF, ikafika mahali wakaonyesha ukarimu wa ajabu chini ya Hamad Rashid, Mbunge wa CUF, Wawi, Pemba.
Hamad Rashid kama kiongozi wa kambi ya upinzani aliwapa nafasi Chadema ya kushika nafasi ya umakamu wa kiongozi wa kambi ya upinzani. Dr Wilbroad Slaa akapewa mikoba hiyo na akawa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge wa Hesabu za Mashirika ya Umma.
Ajabu ya mwaka 2010, ni pale Chadema, baada ya kupata viti vingi Bungeni, Kamati Kuu ya Chama hicho ikaelekeza, kuwa Freeman Mbowe na Chadema, peke yao, waunde Kambi Rasmi ya upinzani bungeni, ni kwa vile kanuni ziliwaruhusu.
Hamad Rashid wa CUF na David Kafulila wa NCCR- Mageuzi walipatwa na mshtuko na wakaamua kuingia msituni kupambana na Chadema. Wakiwa ‘ Porini’ kisiasa Hamad Rashid na David Kafulila wakamwandikia Spika barua ya kuomba Bunge litengue kanuni ya 131 ili kuruhusu kuundwa kwa Kambi ndogo isiyo rasmi ya upinzani.
Kwa Spika Anne Makinda, ambaye moyoni angetamani hata hiyo Kambi rasmi ya upinzani isiwepo, ombi la CUF na NCCR kuongeza kambi nyingine halikumpa tabu kulitupilia kapuni, kwa maelezo ya ‘ Kibunge’;
“ Kanuni Haziruhusu!”
Swali:
Nini faida basi ya kuwa kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni?
Jibu;
Kiongozi wa Upinzani Bungeni ni mtu muhimu sana. Huyu huunda Baraza lake la Mawaziri. Hawa ni mawaziri vivuli. Mtu huyu hupewa ofisi yake na bajeti yake yenye safari za nje ya nchi pamoja na marupurupu mengine.
Ndiye hupewa nafasi ya kwanza kujibu hoja za zinazowasilishwa na Serikali.
Naam, ni mtu anayehudumiwa na Serikali na hulindwa na Vyombo vyake. Hata gari lake huwa na namba rasmi; KUB- Kiongozi Wa Upinzani Bungeni.
Kama ni ndani ya upinzani, nani asiyetaka kuwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni?