Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Heche John, ameonesha dhamira yake ya kuendelea kupigania mustakabali wa chama hicho na Taifa kwa ujumla.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter) leo Jumanne Desemba 31, 2024,
Heche ameandika ujumbe mzito akisisitiza umuhimu wa CHADEMA kama taasisi muhimu kwa maslahi ya taifa na wananchi wa Tanzania.
“Tuna taasisi ya kuilinda, tuna nchi ya kutetea, tuna Watanzania wa kupigania. CHADEMA ikifa madhara yake ni makubwa mno kwa nchi yetu,” aliandika Heche.
Katika ujumbe huo, Heche amemuelezea mwanasiasa mashuhuri na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara Tundu Lissu, kama kiongozi mwadilifu, mkweli, na mwenye uwazi wa hali ya juu.
“Lissu sio muongo ni mkweli, muadilifu na muwazi,” aliandika, akionesha imani yake kubwa kwa Lissu.
Lissu, ambaye kwa sasa ni mmoja wa wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, ameendelea kuungwa mkono na viongozi na wafuasi wa chama hicho.
Uchaguzi wa nafasi hiyo unatarajiwa kufanyika Januari, 2025, na unatazamwa kama moja ya matukio muhimu katika historia ya chama hicho.