Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (uvccm_tz) taifa, Jokate Mwegelo, amefanikisha ujenzi wa Kanisa Katoliki Kigango cha kijiji cha Tanga, kilichopo Jimbo la Mbinga, Mkoani Ruvuma, katika kijiji cha nyumbani kwa marehemu baba yake, Mzee Ndunguru.
Ujenzi wa kanisa hilo umefanikiwa baada ya Jokate kusimamia zoezi la harambee kwa ajili ya kuendeleza mradi huo, na yeye binafsi kuchangia kwa nguvu zake mnamo mwezi Desemba, mwaka 2023.
“Tunapomaliza mwaka huu wa 2024, ni vizuri kusema sifa na utukufu ni kwa Mungu wetu. Sikuwahi kuwaza ningeweza kushiriki katika ibada hii ya sadaka na kujenga kanisa la viwango hivi kijijini kwetu, mahali alipolala marehemu baba yangu. Natumai Baba yangu anajivunia na namuombea mtoto wangu wa kike, Fionna, awe mtu wa kumcha Mungu na kumkimbilia Mungu aliye hai siku zote za maisha yake. Chanzo cha uhai wetu ni Mungu, nimeanza kurudisha kwa Mungu, kwani vyote tulivyonavyo ni mali yake. Bila Mungu, mimi siyo kitu, si lolote, siyo chochote,” alieleza Jokate.
Jokate amwendelea kumshukuru Baba Askofu Ndimbo kwa uongozi na usimamizi wake mzuri katika ujenzi wa kanisa hilo.
Amwwashukuru pia mafundi, wanakijiji wa Tanga, Mbinga, na ndugu na jamaa zake kwa mchango wao.
Amesema, “Mbao za benchi zaidi ya nusu zimetoka kwenye miti aliyopanda mzee wangu alipokuwa hai hapa kijijini, na ina ubora mzuri sana, zaidi ya miaka miwili bila kukatwa wala kuwekewa dawa, lakini haikuharibika. Hivi sasa tumetumia mbao hizo kutengeneza benchi za kanisa.”.