Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Willibrod Slaa, ametoa rai ya wazi kwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe , kujitafakari na kuachia nafasi ya uongozi ili kutoa nafasi kwa kizazi kipya cha viongozi kama Tundu Lissu .
Related Content
Dkt. Slaa ametoa maoni hayo akizungumzia medani za kisiasa za sasa, akisisitiza kuwa nyakati zimebadilika na zinahitaji mbinu mpya na viongozi wapya wenye uwezo wa kukabiliana na serikali ya CCM kwa ujasiri na ukali wa hoja.
“Kila mtu anatakiwa katika mapambano kwa wakati fulani. Leo si wakati wa Mbowe. Miaka 30 ya uongozi wake imemaliza mchango wake mkubwa, lakini sasa taifa linahitaji watu tofauti kama Lissu na Heche ambao hawamung’unyi maneno,” amesema Dkt. Slaa katika mazungumzo yake ya hivi karibuni.
Akifafanua zaidi, Dkt. Slaa amesema kuwa mbinu za kisiasa zilizofanikiwa chini ya uongozi wa Mbowe hapo awali zimepitwa na wakati. Hii ni kutokana na mabadiliko makubwa katika mfumo wa siasa na ujasiri unaohitajika leo kukabiliana na utawala wa CCM.
Dkt. Slaa amesisitiza kuwa Tanzania ya sasa inahitaji viongozi wenye msimamo mkali na wa moja kwa moja dhidi ya CCM.
“Mbowe ni mtu wa ku-compromise, lakini leo hatuhitaji compromise. Tunahitaji viongozi wa aina ya Lissu na Heche ambao wanaweza kuikemea CCM kwa lugha kali, lakini si ya matusi,” amesema.
Kwa mujibu wa Dkt. Slaa, hotuba za Mbowe za hivi karibuni hazijawahi kuikemea serikali kwa namna ambayo inawapa wananchi ujasiri wa kusimama dhidi ya CCM.
“Mbowe amefanya kazi kubwa kama Musa alivyowatoa waisraeli utumwani. Lakini kama Musa hakuingiza watu wake Kaanani, Mbowe pia anapaswa kukubali kazi hiyo iendelee na kizazi kipya cha viongozi”, amesema Dkt. Slaa.
Dkt. Slaa ametoa onyo kali kuwa kwa mtindo wa sasa wa uongozi wa Mbowe, CCM itabaki madarakani hadi 2050.
“Tanzania inahitaji viongozi wapya wenye silaha mpya za kisiasa. Mbowe hana uwezo wa kumwondoa Rais Samia madarakani. Tukimung’unya maneno, tutapoteza taifa zima,” amesema.
Dkt. Slaa alikumbushia mabadiliko ya uongozi ndani ya CHADEMA yaliyofanikisha kupatikana kwa damu mpya katika nyakati tofauti, akiwataja viongozi waliokubali kuachia nafasi zao kama Mzee Edwin Mtei na Bob Nyanga Makani.
“Mzee Mtei alijitoa kwa hiari baada ya kulima shamba la CHADEMA. Mbowe naye anapaswa kufuata mfano huo kwa kuachia nafasi kwa kizazi kipya,” amesema Dkt. Slaa.
Related Content