Kamati tendaji ya Kanda ya Serengeti katika kikao chake cha jana Jumatano Januari 08, 2025 kimefikia maamuzi ya kumvua Uongozi Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Mkoa wa Shinyanga Bw. Emmanuel Ntobi kutokana na utovu wa nidhamu na maadili ikiwemo kuchafua Viongozi wa Chama chake Kitaifa kupitia mitandao ya Kijamii.
Related Content
Akizungumza ma JamboTv Usiku huu (Januari 09, 2025) Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chadema Kanda ya Serengeti Lucas Ngoto ameiambia JamboTv kuwa maamuzi hayo ya Kikao yamefikiwa Kisheria ikiwa ni mara baada ya kumpa fursa ya kuweza kujitetea dhidi ya kauli na maandiko yake kadhaa yasiyokuwa na utu na heshima kwa Viongozi wa Chama Taifa.
Ntobi ambaye pia mwaka 2023 aliwahi kusimamishwa Uenyekiti wake kwa mwaka mmoja kutokana na makosa ya kinidhamu, amejitanabaisha mitandaoni kama muungaji mkono na Mpiga kampeni kwaajili ya Mhe. Freeman Mbowe kuweza kurejea tena madarakani kama Mwenyekiti wa Chadema Taifa, amekuwa na mfululizo wa maandiko kadhaa, yenye nia ya kumchafua, kumtweza na kumtusi Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa Mhe. Tundu Lissu ambaye pia ni Mshindani na mgombea mwenza wa Mhe. Mbowe kwenye nafasi ya Uenyekiti wa Chadema taifa kwenye uchaguzi utakaofanyika baadae mwezi huu.
Miongoni mwa kauli zake ni pamoja na kumuita Makamu mwenyekiti huyo kuwa Mropokaji, Mmbea, sambamba na kumtuhumu kufadhili na kuunda kikosi kilichokuwa kinatumia jina la ” sauti ya wananchi” akishirikiana na watu maarufu mtandaoni na maafisa wa CCM, idara ya usalama wa taifa na Diaspora kwaajili ya kumfitini Mhe. Mbowe
Aidha Ntobi amekuwa akimuhusisha na baadhi ya matendo yasiyofaa kimaadili kupitia maandikio yake akimuhusisha na “Mzungu” hasa pale Mhe. Lissu anapokuwa safarini nje ya nchi kama ” Soon ataweka wazi faragha za Mzungu wake” pamoja na “Si tuliwaambia jamaa yenu kakimbilia kwa mtasha wake? kiko wapi?”, mwisho wa kunukuu.