Wikendi ya Ubaya Ubwela Twende Robo Fainali imefika. Simba ina dakika 90 za kuamua hatma ya kufuzu robo fainali kwa mara nyingine tena katika michuano ya Kombe la Shirikisho kesho Jumapili.
.
Mechi ya kesho kwa wawakilishi hao wa Tanzania ni muhimu kwani ndio itakayotoa dira ya kwenda robo na kama litatokea la kutokea, basi watasubiri hadi wikiendi ijayo kumalizia kazi wakiwa nyumbani, lakini uzito mkubwa ni mchezo wa kesho kwani itafanya mechi ya mwisho isiwe na presha.
.
Ni mechi ya mapema. Itapigwa pale nchini Angola kwenye Uwanja wa 11 de Novembro, Luanda. Wote wawili hapa wana nafasi ya kufuzu. Wanatofautiana pointi tatu tu, Simba iliyopo nafasi ya pili katika msimamo wa kundi hilo ina tisa, wakati wenyeji Bravos yenye alama sita ikiwa ya tatu na kila moja imecheze mechi nne.
.
Ushindi au sare tu, kwa Simba utaifanya ifuzu moja kwa moja robo fainali kutoka kundi hilo, kwani itafikisha kati ya pointi 10 ama 12, lakini kama itapata ugumu kwa Bravos, maana yake kila moja itafikisha pointi tisa na sasa kusubiri mechi za mwisho wiki ijayo kuamua nani aende robo.
.
Simba inapaswa kuwa makini kwani Waangola hao mechi mbili za nyumbani wamegawa dozi mfanano ya mabao 3-2 dhidi ya CS Constantine na CS Sfaxien hivyo inapokwenda kushambulia isisahau kujilinda.