Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bunda mkoani Mara hapa nchini, Karoli Mganga amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma akikabiliwa na mashtaka 178 likiwemo la kuongoza genge la uhalifu.
Mbali na Padri huyo, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni aliyekuwa mhasibu wa kanisa hilo Gerald Mgendigendi.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Jumanne Agosti 6,2024 mbele ya hakimu Mkazi Mfawidhi, Aloyce Katemana na kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Akiwasomea mashtaka hayo, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Mara, Amoscye Erasto amedai walitenda kosa la kughushi nyaraka, kinyume cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Amedai washtakiwa hao wakiwa watumishi wa kanisa hilo, waliiba bilioni sh. Bilioni 7 pamoja na fedha za kigeni, ikiwepo dola zaidi ya 100,000 na Euro zaidi ya 20,000.
Amedai jumla wanakabiliwa na mashtaka 178, yakiwepo ya kuongoza genge la uhalifu, utakatoshaji fedha pamoja na mashtaka mengine.
Hata hivyo baada ya kusomewa mashtaka hayo hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo itatajwa tena Agosti 20,2024 na baada ya kusomewa mashtaka hayo wamepelekwa rumande.