Na; mwandishi wetu
Mwanasiasa mkongwe hapa nchini na mmoja wa waasisi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mzee Pius Msekwa ametoa wito kwa vyama vya upinzani nchini kutumia muhimili wa Mahakama kufikisha kilio na malalamiko yao kwenye maeneo ambayo wanaona hawakuridhika na hawakutendewa haki katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 uliohitimishwa mwishoni mwa mwezi uliopita
Msekwa ambaye pia amewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa ushauri huo wakati akichangia kipindi cha mjadala wa kila wiki cha maoni kinachoandaliwa na kurushwa na shirika la habari la kimataifa la Ujerumani (DW) kupitia idhaa yake ya kiswahili, ambapo katika maoni yake mstaafu huyo alianza kueleza endapo amefurahia ushindi wa asilimia 99 iliyopata chama chake (CCM) katika uchaguzi huo
“Hapana, palipo na malalamiko mtu mwenye akili timamu hawezi kufurahia hali hiyo, watu wazima kama mimi tunafurahia pale ambapo hakuna malalamiko, uchaguzi unafanyika hakuna malalamiko aliyeshindwa anakubali na aliyeshinda anaendelea na sherehe zake, lakini muhimu ni kukumbuka kwamba kazi ya kutunga sheria za uchaguzi imeweka nafasi ya malalamiko ili ambaye hakuridhika aende Mahakamani, nafasi hiyo iliwekwa kwa kuwafikiria wale ambao wataonewa, na hiyo sheria imekuwepo tangu uchaguzi wa kwanza wa uhuru na imekuwa ikitumika, ambapo walalamikaji walikuwa wanaenda Mahakamani” -Msekwa
Akizungumzia ushindi wa asilimia 99 iliyopata chama tawala (CCM) katika uchaguzi huo, Msekwa amesema ushindi huo umetokana na mambo mengi miongoni mwake ni pamoja na vyama vya upinzani nchini kushindwa kusimamisha wagombea kwenye kila nafasi
Kuhusu madai yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba hivi karibuni kuhusu matumizi ya vyombo vya dola kwenye masuala ya siasa, Msekwa amesema kwa ufahamu wake na kwa ushahidi wa macho yake hajawahi kushuhudia jambo hilo, na hata kwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa ndio kwanza amesikia madai hayo hivi karibuni
“Ndio maana nasisitiza kwamba, sisi wakati wa zamani tulikuwa tunafanya vizuri kwa kupeleka malalamiko kama haya Mahakamani, Mahakamani kila kitu kinawekwa wazi na ushahidi unawekwa wazi, Mahakama itasema Polisi wa mahali fulani walifanya hili na hili” -Msekwa
“Hili sio jukumu la chama kimoja (CCM pekee) bali hii ni nchi ya vyama vingi, kinachotakiwa ni uvumilivu tu, tukae pamoja, tukae pamoja tukubaliane kwamba hili ndio jawabu, kama Mahakama hazitakiwi, haziaminiki basi tuende kwenye chombo gani ambacho kitatuondoa kwenye tatizo?, mimi point yangu ni kwamba tusikae kulalamika tu bali tutafute jawabu la malalamiko hayo ili kusudi yasiendelee kutokea huko siku za usoni” -Msekwa
Hivi karibuni wakati akizungumza na wanahabari Jaji mstaafu Joseph Warioba alibainisha kasoro lukuki zilizokuwa zimejitokeza kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 ambapo kwa namna moja au nyingine alieleza hatari ya kuvihusisha vyombo vya ulinzi na usalama kwenye michakato ya kisiasa
“Vyombo vya ulinzi na usalama viliandaliwa, waliambiwa mapema wajiandae kuzuia vurugu yoyote itakayotokea, Polisi waliambiwa wajiandae na hata Jeshi (JWTZ) waliambiwa, hii ina hatari kubwa sana, mchakato wa uchaguzi imekuwa kama hali ya hatari kwamba unajiandaa kuna hali ya hatari, unaandaa vyombo vya ulinzi na usalama” -Jaji Warioba
Jaji Warioba alitumia mkutano huo wa wanahabari kukemea vikali matumizi ya vyombo vya dola kwenye michakato ya kisiasa, ambapo akitolea mfano JWTZ alisema Jeshi hilo limefanya kazi nzuri tangu nchi yetu ilipopata uhuru hadi sasa, na kwamba katika nchi yetu kwa sasa JWTZ ndio taasisi pekee iliyobaki ambayo inafanya kazi zake kwa uaminifu, uadilifu, uzalendo na nidhamu.