Na; mwandishi wetu
Mchakato wa uchaguzi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) unaendelea kuchukua sura mpya na kugusa hisia za wengi, huku wadau tofauti wakijitokeza kila uchwao na kueleza msimamo wao kuhusiana na wagombea wa nafasi mbalimbali waliochukua fomu au kutangaza nia ya kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo
Pamoja na mambo mengine, mvutano na mchuano mkali unaonekana kuwepo kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho kikuu cha upinzani hapa nchini, ambapo Mwenyekiti anayemaliza muda wake aliyechukua fomu ya kutetea kiti chake Freeman Mbowe anakabiliana na wagombea kadhaa kwenye nafasi hiyo huku mshindani wake wa karibu akiwa ni Makamu Mwenyekiti wa sasa wa Tanzania Bara Tundu Lissu .
Mkurugenzi mtendaji wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) Bob Chacha Wangwe naye ni miongoni mwa waliojitokeza kutia maneno kwenye mchuano huo ambao kwa mtazamo wake amesema wazi kuwa kwa sasa CHADEMA inamuhitaji zaidi Tundu Lissu kuliko Freeman Mbowe
Bob Chacha Wangwe ambaye pia ni kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ametumia mitandao yake binafsi ya kijamii kuandika maelezo yafuatayo, “Kwa Watanzania na wanamageuzi wenye mapenzi mema na CHADEMA na Taifa letu, kwa vijana wanaotamani kufanya siasa za upinzani kwa miongo kadhaa ijayo Lissu is the way, hawezi kuwa mkamilifu kama binadamu, lakini ana sifa muhimu kwa maslahi ya CHADEMA na Taifa, kwa kizazi hiki watu wa aina yake ni wachache sana, Lissu kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA haiwezi kuwa habari njema kwa watawala, huyu ndiye mtu sahihi”
“Tutakuwa na wakati mgumu sana katika kufanya siasa kama atashinda mtu mwingine zaidi ya Lissu, mfano ikitokea Mheshimiwa Mbowe ametetea kiti chake, kule Bungeni kesho kutwa kina Kibajaji wakipeleka muswada wa kuondoa ukomo wa Urais tutakuwa na hoja gani za kutetea ukomo?, zipo hoja nyingi ambazo tutakosa uhalali wa kuzisemea, tuwaunge mkono tunaowapenda lakini tufikirie pia uendelevu wa chama (sustainability) baada ya uchaguzi” -Bob Wangwe
“Natambua uwezo na mchango mkubwa wa Mheshimiwa Mbowe na nikiri tu tumekuwa na ukaribu kuliko ukaribu wangu na Mheshimiwa Lissu lakini kwa maslahi mapana ya chama ambacho amekijenga kwa gharama kubwa naona Lissu anatosha kabisa kumpokea kijiti cha Uenyekiti hasa kwa wakati huu ambao tuko kwenye matatizo makubwa ya kidemokrasia, morali za watu wetu ziko chini hasa baada ya kuumizwa na mifumo ya uchaguzi, kwa mazingira haya mabadiliko ni muhimu ili kuirejesha” -Bob Wangwe
“Lissu akishinda tutakuwa na timu kamili (Mwenyekiti Mbowe atabaki kuwa Mzee wa chama na Mjumbe wa kudumu wa Kamati Muu ya chama) hivyo, bado atakuwa na nafasi ya kujenga chama, waliorudi nyuma kisiasa naamini watarudi kazini na wasioitakia mema CHADEMA wataona aibu sana, habari ya kuwa ‘neutral’ ni unafiki, mimi niko na Lissu, tufanye kampeni za kistaarabu wote hawa ni viongozi wetu ili tuendelee kutoa somo kuwa chama chetu ni cha kidemokrasia” -Bob Wangwe