HAWATEKI WATU, WANATEKA UHURU WETU.
Nimepata misiba miwili kwa wakati mmoja. Nimefiwa na rafiki yangu kipenzi, hayati Askofu Chediel Sendoro. Thamani ya urafiki wetu ilijengwa katika kuvumiliana.
Msiba wa pili, nimefiwa na taifa langu ninalolipenda na kulitumikia kwa moyo wangu wote. Watu wanaojulikana na kujifanya hawajulikani, wameuteka uhuru na amani ya taifa langu. Wanadhani wanateka watu, wakosoaji, wachochezi, wapinzani nk lakini kimsingi wanateka uhuru na amani ya taifa letu. Taifa bila uhuru, linakuwa mfu na ni sawa na kipande cha ardhi tu.
Nimefiwa. Natafakari haya:
- Mwaka 2001 tulipata wakimbizi baada ya uchaguzi mkuu kule visiwani. Hayati Ben Mkapa alijutia tukio lile kabla ya kifo chake. Raia kukimbia nchi yake si jambo la kujivunia. Nimewahi kuwa mkimbizi, sipendi mtu mwingine awe mkimbizi.
- Baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2009 na uchaguzi mkuu wa 2020, tulipata tena wakimbizi walioondoka. Ujio wa Rais Samia uliwarudisha nchini. Tuhitimishe kupeleka wakimbizi wengine nje. Tupeleke bidhaa mnadani siyo watu wetu. Anayependa wakimbizi aende yeye.
- Nchi zote zilizowahi kupitia hali tuliyoipitia mwaka 2020, kama vile Ujerumani, Rwanda, Bosnia na kwingineko zina kitu zinafanana. Hujiapiza kuwa ISITOKEE TENA. Hatukujiapiza tulipoanzisha 4R’s. Kamati ya Maridhiano, Tume ya Mkandala, na Tume ya Haki Jinai havijatusaidia. Tujaribu “Gachacha” ya Rwanda au Tume ya Ukweli na Maridhiano (TRC) ya Afrika Kusini. Tujiapize kitaifa, ISITOKEE TENA.
- Wanaosema SAMIA MUST GO ni sawa na waliosema ATAKE ASITAKE. Yote ni kuvunja katiba. Tuliwavumilia wale; Tuwasikilize hawa. Maneno matupu hayavunji mfupa. Waliposema Atake Asitake, ilikuwaje?
- Matumizi ya nguvu hayana faida kwa wote. Kwa mwenye dola ni sawa na kuvunja vikombe halafu ukagharimika kuvinunua tena baada ya ugomvi. Kwa asiye na dola ni kutozwa kodi kulipia vikombe vilivyovunjwa. Kutumia nguvu ni kutangaza kushindwa; haina tofauti na kubaka baada ya kukataliwa penzi. Acheni ubakaji.
- Uhuru ukipotea hakuna aliye salama. Ukitumika kuua, aliyekutuma hatakuamini tena. Atatuma wa kukuua ili awe salama na mnyororo hautaisha. Sisi ni ndugu moja, TUSITEKANE na TUSIUANE. Wanaolindwa ni mateka wa walinzi wao. Tuulinde uhuru kwa gharama yoyote. Wote tutafaidi.
- Uhuru ulipotekwa mwaka 2020; mihimili yote iliumia. Bunge la chama kimoja hata waliomo hawalipendi. Halmashauri za chama kimoja hata mchwa hawazipendi. Uhuru wa mahakama ulitekwa ukabakia wa maandishi. Waliotekwa awamu ya tano wakajikuta ni watekaji wa awamu ya sita. Zipo dalili za kuteka demokrasia mwaka 2024 na 2025. Taifa la fikra moja nani analitaka?
- Kinachoshangaza sasa: Hakuna tofauti ya “ukamataji na utekaji”. Ikiandikwa “tumemkamata”, mashuhuda wanasema “ametekwa”. Waliokamatwa na waliotekwa wakati ule, tuliambulia viroba. Kwa nini tunatumia fedha nyingi kufundisha watu kukamata halafu wakaishia kuwa watekaji?
- Mauaji si lazima yawe ya wengi. Hata mmoja ni wengi kwa sababu kuna wazazi wamejaliwa mtoto mmoja tu. Mtoto mmoja wa wazazi hao ndio watoto wao wengi. Tusirahisishe damu ya mwanadamu kwa sababu haina bei. Katika kila binadamu kuna u-Mungu ndani yake. Tusimuue Mungu!
- Agizo la uchunguzi limetolewa. Kujichunguza ni kugumu; Rais Samia aliwahi kusema. Kelele za wanaohoji uchunguzi ni sawa na kelele za waombolezaji. Waliopiga wamemaliza kazi yao. Wanaolia wasichaguliwe namna ya kulia. Namwogopa sana anayepigwa bila kulia kuliko anayelia bila kupigwa.
Kwa dhamiri safi na sadaka kwa taifa langu.
Wakristo huwa tunaimba, “vingine vyote chukueni, niachieni Bwana Yesu”.
Watanzania wa itikadi zote, dini zote na hali zote tuimbe, “vingine vyote chukueni, tuachieni uhuru wetu wa kufikiri, kusema, kukusanyika, kuabudu na kupumua”.